Huduma ya bure ya upasuaji wa moyo THI
Muungano wa nchi za Falme za Kiarabu kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa moyo kutoka nchi mbalimbali duniani wameanza kutoa huduma ya upasuaji wa moyo bure katika Taasisi ya Moyo Tanzania (THI) iliyopo jijini Dar es Salaam
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Balozi wa Falme hizo hapa nchini, Mallalla Mubarak, amesema nchi yake imetoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo hivyo matibabu yatatolewa bure THI na huduma hiyo itadumu kwa wiki mbili kuanzia tarehe 17/10/2008 hadi 31/10/2008, na amewataka Watanzania wote, watoto kwa wakubwa wenye maradhi hayo kuhudhuria katika hospitali hiyo iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Amesema, wananchi wengi wanaokabiliwa na maradhi ya moyo wanakufa kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu nje ya nchi.
Balozi Mubarak amesema wananchi wote wenye matatizo ya moyo wanatakiwa kufika hospitalini hapo ambapo watawakuta madaktari bingwa wakiwasubiri.
Aidha, amesema kwa kuanza watafanya kazi ya kuwachunguza wagonjwa wote watakaofika hapo baadaye kazi ya upasuaji itaanza.
Amefafanua kuwa madaktari bingwa watakaoshiriki katika upasuaji wanatoka Uingereza, Misri, Ufaransa, India na wengine kutoka hapa nchini.
Ameongeza kuwa utafiti uliofanywa na nchi yake hapa nchini umebaini kuwa watu wengi wana matatizo ya moyo.
Amesema baada ya kumaliza uchunguzi wa awali wataanza kutibu wagonjwa watakaobainika kusumbuliwa na moyo.
Balozi huyo amesema, licha ya mgonjwa kufanyiwa matibabu ya moyo pia atapatiwa dawa zingine bure,na zoezi hilo pia litafanyika visiwani Zanzibar na Pemba.
Nchi ambazo tayari mpaka sasa zimenufaika na ufadhili huo ni Kenya, Sudan, Ethiopia, Syria na Morocco.
Naye Mkurugenzi wa THI, Dk. Ferdinand Masau, amesema zoezi hilo litachukua wiki mbili na kipindi hicho kila mtu anayesumbuliwa na moyo afike kwa ajili ya kupata matibabu bure.
Dk. Masau amesema watakuwa wanatoa huduma hiyo kwa watu 15 kwa siku wakiwemo watoto na watu wazima.