|
Kituo cha Afya Nyakato
Kituo cha Afya Nyakato na matumizi ya TEKNOHAMA.
Kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) kumeleta mafanikio makubwa katika sekta ya afya nchini Tanzania, ambapo huduma hiyo imeboreka kwa kiwango kikubwa kwa baadhi ya hospitali,vituo vya afya na Zahanati ambazo zinatumia mfumo huo katika kutoa huduma. Kituo cha Afya Nyakato kilichopo jijini Mwanza, ambacho kinamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT),Dayosisi ya ziwa Victoria,kinatumia teknolojia hii katika kutoa huduma ambapo kimefanikiwa kwa takribani asilimia 80 kuifanya huduma hiyo kuwa bora zaidi na kuleta chachu ya Maendeleo kituoni hapo kwa kutoa huduma ya haraka kwa watu wanaopata tiba katika kituo hicho.
Dkt.Bonaventura Mazezele Mganga Mfawidhi wa kituo hicho anasema Teknolojia hiyo ya matumizi ya Kompyuta imeanza kutumika kituoni hapo kuanzia mwaka 2006 kwa baadhi ya idara kama vile Mapokezi na Ofisi ya Mganga Mkuu.
Mwaka 2007 ndipo teknolojia hiyo ilipoanza kutumika rasmi baada ya kuanza kutumia “Software” (Programu)ya Afya-pro ambayo imetengezezwa maalumu kwa matumizi ya hospitali ambayo inahifadhi taarifa za Mgonjwa,Takwimu pamoja na data. Software hii ambayo .imebuniwa na Kampuni ya Teknolojia (NPK) ya jijini Dar es salaam,mbali ya kuwa na uwezo wa kuhifadhi taarifa za Mgonjwa na takwimu, pia ina uwezo wa kuendesha stoo ya madawa ambapo inamwezesha msimamizi wa stoo kujua kirahisi idadi ya dawa zilizopo stoo na zile ambazo zimekaribia kuharibika, inauwezo wa kumpa taarifa mhusika kuwa aina fulani za dawa zimekaribia kuisha hivyo ajiandae kuagiza zingine.
Dkt.Mazezele anasema, hapo mwanzo kabla ya kuanza kutumia mfumo huo utendaji kazi ulikuwa mgumu, kwani kazi nyingi zilifanyika kwa njia ya mikono,kadi za wagonjwa utunzwaji wake ulikuwa si mzuri na nyingi ziliharibika,wagonjwa walichukua muda mrefu kumuona Daktari kutokana na foleni kubwa iliyokuwepo,usimamizi wa madawa na uandaaji wa ripoti ilikuwa ni tatizo kubwa kwani ripoti zilichukua wiki nzima kuandaliwa, upotevu wa mapato ulikuwa mkubwa, kwa ujumla kazi likuwa ni ngumu.
Daktari anasema baada ya mfumo huo kuanza kutumika kituoni hapo wamepata mafanikio makubwa ambapo kazi za mikono (paper work) zimepungua, kwani mfumo huo kwa sasa unatoa ripoti haraka na kuzalisha kadi za wagonjwa,unahifadhi taarifa za mgonjwa kirahisi na kutunza data,mapato yameongezeka,idadi kamili ya wagonjwa wanaofikia kituoni hapo kupata tiba inafahamika kirahisi.
Pamoja na mafanikio hayo,Dkt.Mazezele anasema kuna mapungufu machache ambayo bado yanawakabili ili kuifanya huduma hiyo iwe bora zaidi.Ameyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na upungufu wa kompyuta, kompyuta zilizopo hatoshi,hivyo anaomba mamlaka husika kulifanyia kazi suala hilo.
Imewekwa: 27th Nov 08 na Renatus J Sona
|