Mafunzo ya uwezeshaji
Baadhi ya wafanyakazi wa miradi inayofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano na Maendeleo (IICD) la nchini Uholanzi, wamepewa mafunzo ya uwezeshaji katika kuboresha shughuli zao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Nyakahoja jijini Mwanza yalihusisha watumishi wa hospitali katika idara za Mapokezi na Maabara,yalilenga kumjenga muhusika kujitambua, kujiamini na kuwa na uwezo wa kuongoza warsha, semina na kuhudumia watu wa aina mbalimbali.
Katika mafunzo hayo washiriki walifundishwa sifa za kuwa mwezeshaji mzuri ambazo ni pamoja na kuwa na maandalizi ya kutosha kabla ya kufanya kikao au Semina,kufuata utaratibu katika kuongeza semina, kuwa mbunifu katika kazi, kusoma hadhira uliyonayo na kuielewa, kujenga mahusiano na washiriki wengine na kutumia lugha inayoeleweka.
Mafunzo hayo ya siku tano yalihusisha washiriki kutoka Mradi wa kuhifadhi taarifa za afya kwa kutumia Kompyuta (DHMIS), AfyaMtandao na wengine kutoka hospitali za Bukumbi, Kituo cha afya Nyakato ELCT, Zahanati za Makongoro na Nyakahoja.
Kwa upande wao washiriki wameshukuru kwa mafunzo hayo na kuahidi kuwa watatumia ujuzi walioupata kuboresha kazi zao,pia kuwashirikisha wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika mafunzo.