|
CSSC na huduma ya afya
CSSC na mkakati wa utoaji huduma ya afya kwa njia ya mtandao Deogratius Temba
UNAPOSEMA neno ‘mtandao’ ni dhahiri unazungumzia kuhusu teknolojia mpya inayotumia mifumo ya mawasiliano ya kompyuta yaani intaneti, barua pepe na mawasiliano mengine yaliyoko kwenye mifumo hiyo.
Ni wazi kuwa ulimwengu umeanza kubadilika na hata kulazimisha kila kitu kwenda sambamba na mifumo hiyo na kuingizwa katika mitandao. Na kurahisha kazi, muda na gharama kutokana na uharaka wa kufanya jambo.
Kupitia Mfumo wa intaneti shughuli zote huenda na wakati na kuharakisha kupata majibu pale unapokuwa umeuliza swali. Mfano, ni rahisi kuwasilina na mtu akiwa Ulaya au Marekani kwa muda mfupi na kupata majibu.
www.afyamtandao.org ni mtandao wa kompuyta ulioanzishwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), kwa lengo la kuunganisha hospitali zote za CSSC katika mtandao tarakilishi ili kuwezesha ukusanyaji, uhifadhi, na upashanaji taarifa. Ikiwa ni pamoja na ubadilishaji wa uzoefu wa maarifa miongoni mwa watumishi wa afya na wadau wengine na sekta ya afya.
Mradi umeanzishwa kwa ufadhili wa taasisi ya kimataifa ya Uholanzi wa mawasiliano na mendeleo (IICD).
Ni sehemu ya mkakati wa CSSC wa kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma za tiba katika hosipitali zake zote nchini kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA).
Ofisa wa Teknolojia ya Mawasiliano wa CSSC, Petro Pamba, anasema chanzo cha www.afyamtandao.org ni mkutano wa pamoja wa washika dau wa sekta ya afya na sekta ya teknolojia ya habari ya mawasiliano.
Mkutano huo uliofanyika Mwanza, Februari 2005, ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuwezesha matumizi ya TEKNOHAMA katika mfumo wa taarifa za uendeshaji wa shughuli za afya katika ngazi za wilaya.
Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, CSSC, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kwa ushirikiano na IICD, na Shirika la Netherlands Catholic Organization for Relief and Development Aid (CORDAID).
Baada ya hapo mradi huo ulianzia huko Mwanza na tayari hospitali zote za wilaya za mkoa huo zimeingizwa kwenye mfumo huo. Hospitali za wilaya za Magu, Sengerema, na Nyamagana, ambazo sizingeweza kufikika kwa urahisi, sasa watumishi wa afya hasa madaktari wameanza kujifunza na kutumia mitandao hii na wanazidi kuelimishwa na kushauriwa kubadilika.
Hii itawafanya waweza kufanya mawasiliano ya kimtandao na madaktari wengine bingwa, moja kwa moja ndani na nje ya nchi kwa kutumia mtandao na kupata maelekezo namna ya kumuhudumia. Ukiwa katika mtando huu, wadau wa sekta ya afya wanaweza kufanya huduma zao kwa ufanishi zaidi bila ya kumuhamisha mgonjwa kutokana hosipitali moja kwenda nyingine.
Mfano mgonjwa wa saratani anaweza kutibiwa Mwanza kwa kutumia mtandao huu, bila ya kwenda Dar es Salaam, kuhudhuria kliniki ya Saratani katika taasisi ya Ocean Road au nchini India waajili ya upasuaji wa moyo.
Daktari anayetumia mtandao ataweka historia na rekodi na hata picha za mgonjwa wake kwenye mtandao na taarifa za kila siku, atauliza maswali, ambayo madaktari bingwa walio kwenye mtandao watamjibu na kumwelekeza dawa za kumpa mgonjwa huo.
CSSC wanaeleza kuwa mradi huu ni muhimu ukatumika pia kwa kuwafundisha wanafunzi wa Chuo cha Afya wa Sengerema. Hospitali iliyo nje kabisa ya jiji la Mwanza, sasa wanaweza kushiriki kipindi pamoja na wanafaunzi wa Chuo cha Tiba cha Muhimbili, kupitia mtandao kama huo.
Hata hivyo wafanyakazi wa sekta ya afya wanahitaji kujifunza na ni lazima kuwa wa kisasa kwa kuendana na wakati hata kwa wale walioko vijijini.
Kwa kutumia mtandao huu, na njia ya elimu kwa kwa mtandao (eLearning), wanaweza kujifunza mambo mengi. Kutumia njia ya eLeaning, wanaojifunza wanaweza kupata elimu kupitia diski (CDs), simu za mkononi, au intaneti ambayo itawawezesha kurahisisha kazi.
Mratibu wa elimu mtandao (eLearning), Dk. Denis Mazali, anasema anasema Tanzania imechelewa kujiunga na mfumo huo wa kutoa elimu kupita mtandao. Sekta ya Afya inashida kutokana na watu wengi kutokuwa tayari kubadilika na kuingia kwenye mfumo mpya wa Mtandao kwa kila kitu. CSSC wanasema mtu binafsi anaweza kujiunga na afya mtandao kwa lengo la kuilinda afya yake binafsi.
CSSC ni chombo kilichoundwa mwaka 1992 kwa pamoja kati ya Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), kwa lengo la kusimamia huduma za afya na elimu zinazotolewa na makanisa hapa nchini. Ni chombo kikubwa Afrika ya Mashariki kwa vuile kina dayosisi na majimbo 87 na kinamiliki na kuendesha asilimia 40 ya huduma za afya na asilimia 24 ya huduma za elimu zitolewazo hapa nchini.
Imewekwa: 11th Mar 09 na Renatus J Sona
|