|
Mfumo wa taarifa za rasilimali watu (HRIS)
Warsha ya mfumo wa taarifa za rasilimali watu Mradi wa Intrahealth/Capacity unaosimamiwa na shirika la USAID la nchini Marekani kwa kushirikiana na shirika la Afya duniani ofisi ya Tanzania (WHO) na Benki ya dunia, kwa pamoja waliandaa warsha ya siku nne ya mfumo wa taarifa za rasilimali watu kanda ya Afrika, warsha ambayo ilifanyika mkoani Arusha hivi karibuni.
Tume ya Kikristo ya huduma za jamii (CSSC) kupitia kitengo cha AfyaMtandao ilikuwa miongoni mwa waalikwa waliohudhuria warsha hiyo. Katika warsha hiyo mambo kadhaa yalijadiliwa yakiwemo kushirikishana uzoefu na kuona jinsi gani takwimu zinavyotumika katika kutoa maamuzi, kuimarisha mtandao wa kanda ambao utajenga utamaduni wa kutumia taarifa kuelezea sera na maamuzi ya kiutawala, kuboresha uwiano baina ya mfumo wa taarifa za afya na mfumo wa usimamizi wa taarifa za afya sambamba na mfumo wa taarifa za rasilimali watu (HRIS).
Pamoja na majadiliano, pia washiriki walipata uzoefu na changamoto zitokanazo na mfumo huo kutoka kwenye nchi za Rwanda na Uganda, usimamizi wa awali wa railimali watu,jinsi ya ukusanyaji taarifa, usimamizi na namna ya mtiririko wa taarifa unavyotakiwa, pia majadiliano jinsi ya kuandaa ripoti kupitia mfumo huo na hatua zinazotakiwa katika kuanzisha na kusimamia mfumo huo.
Katika majumuisho ya majadiliano ilikubaliwa kuanza kutumia mfumo huo kwa wale ambao bado hawajaanza na kupunguza matumizi ya kazi za mkono (manual works) kwa njia ya kujaza mafaili bila kutumia kompyuta, pia kila nchi ihakikishe inasimamia na kufanya tathimini ya maendeleo ya rasilimali watu, Sera ya afya ya rasilimali watu na maendeleo ya mpango mkakati ili mfumo huo (HRIS) uweze kuingizwa katika mpango huo, Kuwepo na msaada wa mafunzo ya kiufundi na utekelezwaji wake.
Baada ya kuona uzoefu utokanao na mfumo huo katika warsha hiyo, mradi wa Capacity Tanzania kupitia Shirika la msaada la Marekani umeonyesha nia ya kuendeleza juhudi zinazofanywa na Tume ya kikristo ya huduma za jamii (CSSC) katika kusaidi kuboresha mfumo huo wa (HRIS) na kuwa sehemu ya mfano kwa Tanzania. Mfumo wa taarifa za rasilimali watu ni mfumo wa kisasa ambao unahifadhi taarifa na takwimu za watumishi katika vituo vya afya, hospitali na zahanati, ni mfumo unaowezesha kujua taarifa mbalimbali za watumishi hao ikiwa ni pamoja na elimu zao, idadi na idara wanazofanya kazi.
Washiriki 58, kutoka nchi za Uganda, Botswana, Lesotho, Swaziland, Rwanda, Namibia na wenyeji Tanzania walihudhuria mkutano huo.
Imewekwa: 5th Jun 09 na Renatus J Sona
|