|
Tathimini ya mradi wa Tibamtandao
Mkutano wa tathimini ya mradi wa TibaMtandao Mradi wa TibaMtandao (Telemedicine) ambao unaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)-Arusha kupitia ufadhili wa Shirika la IICD, uliandaa mkutano wa kushirikishana uzoefu na kiwango jinsi mradi huo unavyotumiwa na wataalamu wa sekta ya afya katika kuboresha utoaji wa huduma ya afya kwenye taasisi za kidini (FBOs) ambazo zinatekeleza mradi huo.
Mkutano huo wa siku moja ulikutanisha washiriki 17 kutoka FBOs, Tume ya Kikristo ya huduma za jamii (CSSC) na wawakilishi kutoka wizara ya mawasiliano sayansi na teknolojia.
Katika mkutano huo mada mbalimbali zilijadiliwa huku lengo kuu likiwa kuboresha mradi huo kwa kufanya uhamasishaji zaidi ili wataalamu wengi hasa madaktari kujinga na kuanza kutumia teknolojia hiyo.Kwa upande wa tathimini, washiriki walizungumzia historia ya mradi, watumiaji wa teknolojia hiyo, motisha kwa watumiaji wanaoshiriki katika mradi, masafa na ubora wa utumiaji wa huduma hiyo na matokeo ya maendeleo ya mradi huyo tangu ulipoanzishwa 2008.
Washiriki kupitia majadiliano walibaini kuwa; asilimia kubwa ya madaktari na watumishi wengine wa afya wanaoshiriki katika Tibamtandao ni wale wenye umri kati ya miaka 21 hadi 40 ambao ni asilimia 61 na wale wenye miaka kati 41 hadi 60 ni asilimia 39 tu.Takwimu pia zinaonyesha kuwa asilimia 67 ya watumiaji ni wanaume na 33 wanawake, ambapo asilimia 78 ni kwa wale wenye elimu ya juu na asilimia 22 ni wale wenye elimu ya sekondari.
Kutokana na takwimu hizo, imeonekana kuwa watumishi ambao bado hawajapata muamko wa kutumia Tibamtandao waendelee kuhamasishwa kwa kujifunza umuhimu wake kutoka kwa wale ambao wanashiriki katika tiba hiyo. Pia ili kuboresha zaidi huduma hiyo imeshauriwa kuwa wahusika wanaopokea taarifa za wagonjwa kwa kutakiwa kutoa ushauri (Consultation), waweze kufanya hivyo haraka ili kusaidia wagonjwa kwa muda muafaka.Pia imeshauriwa kwa watumishi wa afya kutumia Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) kupitia Tibamtandao kama njia bora na ya haraka ya kuboresha huduma ya afya, kufanya hivyo kutapunguza wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta tiba za hospitali kubwa na hata za rufaa.
Kwa kuzingatia umuhimu wa Tibamtandao, imeonelewa kuwa juhudi zaidi zinatakiwa kuwekwa ili huduma hiyo ipanuke zaidi kwa kufika hospitali nyingi hasa za maeneo ya vijijini ambapo itawahamasisha wataalamu wengi wa afya kushiriki na kupata mafunzo ya awali namna ya kufanya tiba hiyo.
Tibamtandao ni mfumo mpya wa maendeleo katika sekta ya afya ambapo teknolojia mpya ya mawasiliano inawawezesha madaktari katika maeneo ya vijijini kupata msaada wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali za rufaa ambao unasaidia kupata ufumbuzi wa tiba halisi inayotakiwa kwa mgonjwa. Mgonjwa anapata huduma ya matibabu sehemu yeyote ile alipo bila ya kusafiri kwenda katika hospitali za rufaa, pia tiba hii inasaidia kuongeza maarifa na utaalamu kwa daktari baada ya kupata ushauri wa tiba kutoka kwa daktari mtaalamu wa tatizo husika (specialist).
Imewekwa: 5th Jun 09 na Renatus J Sona
|