|
Maabara ya kutengeneza ARV
Maabara ya kutengeneza ARV yazinduliwa MUHAS Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba Muhimbili (MUHAS), kimezindua maabara ya mafunzo ya utafiti na kutengeneza dawa, kwa ajili ya kuboresha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa famasia kwa malengo ya kutengeneza dawa ili kupunguza uagizaji kutoka nje.
Maabara hiyo ya kisasa itakuwa ikitengeneza dawa za aina mbalimbali kama vile ARV kwa ajili ya kuwaongezea siku wagonjwa wa UKIMWI, Paracetamol kwa ajili ya kutuliza maumivu na vidonge vingine jambo ambalo litasaidia watanzania kupata dawa hizo kwa urahisi.
Mbali na kutengeneza pia maabara hiyo itafanya vipimo kwa dawa zitakazokuwa zinaagizwa ili kujua kama ni bandia au siyo, ili kuwa na uhakika wa dawa zinazotumiwa na wateja wao.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha kimataifa cha German Action Medeor, Bw.Christopher Bonsmann amesema lengo kubwa la kujenga maabara hiyo ni kujaribu kutengeneza mazingira mazuri kwa wanafunzi na walimu wa MUHAS, ili kujifunza kwa vitendo na kuwapa uwezo wa kuzalisha dawa hata watakapohitimu mafunzo yao.
Ujenzi wa maabara hiyo umefadhiliwa na Serikari ya Tanzania kwa asilimia 55, Ujerumani GTZ kwa kushirikiana na Action Medeor asilimia 30, ambapo asilimia 15 zilikamilishwa na MUHAS kwa lengo la kuongeza ubora wa kutengeneza dawa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Tanzania imekuwa ikiagiza asilimia 80 ya dawa kutoka nje ya nchi na sasa imejipanga kupunguza uagizaji huo kwa asilimia 50.
Imewekwa: 15th Jun 09 na Renatus J Sona
|