|
Hospitali ya Sumve na TEKNOHAMA
Hospitali ya Sumve yafanyiwa tathimini ya TEKNOHAMA Tume ya Kikristu ya huduma za jamii (CSSC) kupitia kitengo cha AfyaMtandao imefanya tathimini ya kubaini mahitaji muhimu yanayohitajika (ICT need assessment) kwa lengo la kuiunganisha hospitali ya Sumve sambamba na chuo chake cha uuguzi katika mfumo wa kisasa wa Teknolojia ya habari na mawasiliano TEKNOHAMA.
Tathimini hiyo iliyofanyika hospitalini hapo hivi karibuni, ilifanywa kwa ushirikiano mkubwa baina ya hospitali yenyewe, Chuo cha uuguzi na CSSC na ililenga zaidi kuainisha maeneo muhimu ambayo wahusika (hospitali na Chuo) wataweza kupata taarifa na habari mbalimbali pia kuchambua aina ya taarifa na habari zinazotakiwa katika tovuti, aina ya teknolojia inayohitajika, kiwango cha utaalamu wa TEKNOHAMA (ICT) kwa watumishi na maeneo muhimu katika mfumo wa kuhifadhi taarifa na rekodi.
Akizungumzia tathimini hiyo mkuu wa mawasiliano ambaye ni mratibu wa kitengo cha AfyaMtandao Bw. Petro Masatu Pamba amesema, katika tathimini hiyo wamebaini kuwa, katika maeneo mengi (vyumba) ya wagonjwa wanaokuja kutibiwa na kuondoka (OPD) kama vile; mapokezi, maabara na malipo tayari kuna Soketi za umeme ambazo zinaweza kuunganisha mfumo mzima wa mawasiliano isipokuwa kwenye maeneo machache kama vile kwenye Bima ya afya.
Bw. Pamba amebainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa Soketi hizo za umeme lakini maeneo hayo hayana Kompyuta hivyo zoezi la kuunganisha litakuwa rahisi. Na katika maeneo ambayo wagonjwa wanalazwa (Wodi), Soketi zipo na zinafanya kazi isipokuwa katika maeneo ya uzazi wa mpango ambapo hakuna mfumo huo.
Na kwa upande wa Kompyuta ni maeneo ya Kliniki kwa waathirika wa Ukimwi (CTC) ambako kuna Kompyuta 2, na 1 ofisi ya mratibu wa masuala ya afya kwa jamii (PHC).Maeneo mengine ambayo kuna Kompyuta ni idara ya Uhasibu, Maktaba na kwa katibu Muhutasi (Personal secretary).Pamoja na maeneo haya kuwa na Kompyuta, hakuna mfumo wowote wa Kompyuta (information system) ambao unatumika katika kuwasiliana kutoka idara moja kwenda nyingine.
Baada ya kufanya tahimini hiyo na kubaini sehemu chache za kurekebisha, hospitali hiyo itaingia katika mfumo mpya na wa kisasa wa mawasiliano ambao utatumia Software ya “Afya Pro” ambayo itaunganisha maeneo muhimu kama vile Mapokezi, Ofisi ya Daktari kiongozi, maabara, uhasibu na katika wodi za wazazi, bima ya afya na madawa.
Mfumo huu utasaidia watumishi kuweza kuwasiliana kirahisi, na mgonjwa kupata huduma kwa haraka pasipo kusubiri katika foleni kwa muda mrefu. Pamoja na kuwa na mfumo huo pia hospitali itaanzisha Tovuti ambayo itakuwa na muudo wa mfumo mmoja wa mtandao (Local area network) ambao utasaidia kuunganisha mawasiliano.
Watumishi watapewa mafunzo ya kutumia mfumo huu pamoja na kompyuta kwa wale ambao hawafahamu.Katibu mtendaji wa hospitali hiyo Sr.Evodia Mwalupagaro, anasema wao kama hospitali wako tayari kuingia katika mfumo huo kwani ni hospitali pekee kubwa katika wilaya ya Kwimba ambayo inahudumia wanachi wengi, kauli hiyo inaungwa mkono na Mkuu wa chuo cha uuguzi cha hospitali hiyo Bi Grace Sahali.
CSSC kupitia kitengo cha AfyaMtandao ni mdau mkubwa katika kuboresha huduma za jamii ambapo kwa sasa imejikita kuhakikisha kwamba hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo ni wadau wake wakuu zinaingia katika mfumo mzuri wa mawasiliano ambao unahifadhi taarifa kwa njia ya Kompyuta.
Hospitali ya Sumve ni hospitali teule ya wilaya ya kwimba ambayo inamilikiwa na Kanisa katoliki jimbo kuu la Mwanza, ilianzishwa na wamisionari wa shirika la “White fathers” na Shirika la masista weupe mwaka 1934.
Mwanzoni hospitali hiyo ilipoanzishwa ilianza kama wodi ya wazazi tu ambapo mwaka 1936 wodi hiyo ilifunguliwa rasmi lakini pia katika mwaka huohuo wodi ya wanaume na jengo la upasuaji (Operation threatre) viliongezwa, ikifuatiwa na kitengo cha meno na mwaka 1939 wodi ya tatu ilifunguliwa pia.
Mpaka sasa hospitali ya Sumve inavyo vitengo 8 vya wagonjwa wanaolazwa (Inpatient department) ambavyo ni wodi za wazazi, akina mama wajawazito, wagonjwa mahututi (ICU), watoto wasiofikisha miezi (Premature ward), wanawake, wanaume, watoto, wagonjwa wa kifua (TB) na wodi ya magonjwa ya kuambukiza (Isolation ward).
Pia hospitali ya Sumve kwa kushirikiana na Cordaid ya Uholanzi imejenga jingo ambalo linatumika kwa wakina mama wajawazito kusubiri muda wa kuingia wodini kujifungua.
Tathimini ya kuunganishwa na TEKNOHAMA ni tathimini ya kwanza kufanywa na CSSC-AfyaMtandao katika hospitali hiyo ambapo tathimini nyingine kama hiyo ilifanyika katika hospitali ya Kolandoto Shinyanga.
Imewekwa: 23rd Jun 09 na Renatus J Sona
|