|
Wizara ya afya na ufafanuzi wa dawa
Wizara ya Afya yakanusha upotevu wa dawa
Na Chalila Kibuda
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imekanusha kuhusu upotevu wa dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kifua kikuu, zinazotolewa na wafadhili wa mfuko wa dunia katika kupambana na magonjwa hayo.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bi.Blandina Nyoni, amesema dawa hizo hazikupotea kama inavyoelezwa bali kulikuwa na uangalizi mbaya.
“Baada ya kupokea malalamiko juu ya upotevu wa dawa hizi, wizara iliwasiliana na mfuko wa dunia na kulazimika kutoa ufafanuzi juu ya matumizi yake kulingana na taarifa ya ukaguzi,’’ alisema Nyoni.
Alisema ripoti ya dawa hizo hazikuweza kupatikana kwa muda mwafaka, kwani zilihifadhiwa kwenye kompyuta ambapo zilipohitajika, hazikuweza kupatikana na kushindwa kuwapatia wafadhili hao.
Nyoni alisema, dola za Marekani 819,000 zilitolewa kwa ajili ya kushughukia magojwa hayo, ambapo tayari Tanzania ilimeingia katika mzunguko wa sita kati ya nane juu ya matumizi ya fedha hizo kama ilivyoidhinishwa na wafadhili.
Hata hivyo amesema, ukaguzi uliofanyika Novemba mwaka 2007, ulilenga kuangalia ununuzi pamoja na usambazaji wa dawa za malaria nchi nzima kwa kupitia mzunguko wa nne, ambao ulilenga ugonjwa wa malaria, uliogharimu dola za Marekani 75,086,764 kwenye manunuzi ya dawa aina ya ALU.
Aidha, amesema kuna dawa ambazo zilipitisha muda katika kila wilaya ambazo zilirudishwa kutokana na ugonjwa wa malaria kupungua kwa asilimia 20.
Nyoni amefafanua kuwa dawa zenye gharama ya dola 819,000 hazikuhesabika kutokana na mtandao wa kompyuta wa Bohari ya Madawa (ORION), ulikuwa na uwezo hafifu katika utendaji ndani ya ukaguzi.
“Naamini kuwa utendaji wa Serikali ya Tanzania kupitia wafadhili ni ufanisi tosha ndiyo maana tutaingia tena katika mkataba mpya hivi karibuni,” alisema Nyoni.
Alisema dawa ambazo zilipelekwa katika vituo vya huduma ya afya, asilimia 27 iliyobaki inaendelea kufuatiliwa ili kupata kumbukumbu muhimu katika kukamilisha hesabu hizo.
Amesema idadi ya wagonjwa wa ukimwi inazidi kuongezeka kila mwaka kutokana na takwimu za mwaka 2004 kuwa na wagonjwa 1,842 hadi wagonjwa 242,290 mwaka huu.
Imewekwa: 7th Aug 09 na Renatus J Sona
|