|
Tathimini ya miradi ya IICD
Tathimini ya miradi inayofadhiliwa na Shirika la IICD Watekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Shirika la kimataifa la mawasiliano na maendeleo la (IICD), wamesema wamelizishwa na misaada inayotolewa na Shirika hilo katika kuboresha huduma ya mawasiliano kwenye sekta ya afya nchini.Huduma hiyo ni ya matumizi ya TEKNOHAMA kwenye sekta ya afya, ambapo inahusisha Kompyuta na mfumo mzima wa kuhifadhi taarifa sambamba na Tibamtandao (Telemedicine).
Watekelezaji hao wamebainisha hayo kwenye tathimini ya kuangalia mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika miradi hiyo ambapo walikutana na kujadili mafanikio na changamoto hizo kwenye mkutano uliyowakutanisha watekelezaji hao uliyofanyika Mwanza hivi karibuni.
Katika tathimini hiyo inaonyesha kuwa asilimia 78 ya uendeshaji wa miradi hiyo inaridhisha ambapo watu wanaotekeleza miradi hiyo wameelezea kuridhishwa na jinsi miradi hiyo inavyotekelezwa, na kwa upande wa utaalamu wa kiufundi na mafunzo, asilimia 70 inaonyesha kuwa mafunzo ya kompyuta yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa kwa walengwa yanarizisha. Pia tathimini hiyo inaonyesha kuwa katika kutekeleza miradi hiyo kuna ushirikiano wa asilimia 91 baina ya watekelezaji wa miradi hiyo na wadau wengine.
Upande wa ubunifu, asilimia 72, inaonyesha kuwa TEKNOHAMA bado ni hitaji muhimu katika sekta ya afya na asilimia 87 ya watekelezaji wa miradi hiyo wameunga mkono teknolojia hii na kutaka izidi kupewa kipau mbele.Pamoja na changamoto kama vile kukatika kwa umeme, upungufu wa vifaa (Kompyuta) na wataalamu wa kutosha, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa matatizo yote haya yanatatuliwa.
Shirika la IICD kwa kushirikiana na Shirika la CORDAID yote ya Uholanzi, yamekuwa yakisaidia miradi mbalimbali ya maendeleao katika kuboresha huduma kwenye sekta ya afya kwa njia ya TEKNOHAMA (Matumizi ya kompyuta).Miradi hiyo ni pamoja na Tibamtandao (Telemedicine), Mfumo wa kuhifadhi na kusimamia taarifa za afya za wilaya kwa njia ya Kompyuta (DHMIS), Mfumo wa Care2x, kituo cha mawasiliano Sengerema (Telecentre), AfyaMtandao, Mafunzo kwa njia ya elekroniki ( E-learning) na mradi E-dispensary.
Imewekwa: 29th Sep 09 na Renatus sona
|