|
Wadau wa afya wavutiwa na mfumo wa Care2x
Mfumo wa kutumia Kompyuta (Care2x) wavutia wadau wengi wa afya.
Wadau wa afya wa kanda ya kaskazini wameelezea mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za afya kwa njia ya Kompyuta (HMIS) unaotumia “Software” ya Care2x, kuwa ni mfumo bora ambao kama ukitumiwa vizuri unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya.
Wadau hao ambao ni madaktari, makatibu afya wa majimbo na wataalamu wa ufundi wa mfumo huo wamebainisha hayo walipokutana kwenye warsha ya siku moja ya kutembelea, kuona na kujadili jinsi mfumo huu unavyofanya kazi katika baadhi ya hospitali za kanda ya Kaskazini.
Baada ya kutembelea mfumo huo, wadau hao walisema mfumo huo ni mzuri na unarahisisha kazi kwa kukusanya taarifa zilizo sahihi hali inayopelekea utoaji wa ripoti kuwa rahisi. Wamezishauri hospitali zingine ambazo hazijaanza kutumia mfumo huo wa Kompyuta kuona umuhimu wake na kuanza kuutekeleza.
Wamesema hospitali ambazo tayari zinatumia mfumo huo ziandae mpango maalumu wa kutoa mafunzo zaidi kwa watumishi wake hali ambayo itapunguza tatizo la kukosa wataalamu wa kutosha wanaojua kutumia Kompyuta.
Akiongea katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Kikristu ya huduma za jamii (CSSC) kanda ya kaskazini kupitia kitengo cha AfyaMtandao kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) kupitia kitengo cha Mawasiliano (ICT-Unit), Msimamizi wa mradi huo Bw. Sunday Morabu amesema Serikali kwa kuona umuhimu wa kutumia TEKNOHAMA (ICT) katika sekta ya afya, imeunda kamati maalumu ambayo inaratibu uundwaji wa Sera ambayo itasimamia masuala yote ya TEKNOHAMA katika sekta ya afya, ikiwemo kuwezesha hospitali, vituo vya afya na Zahanati kuanza kutumia mfumo wa Kompyuta katika kutoa huduma, hali ambayo itaongeza chachu kwa mfumo kama huu kuenea sehemu kubwa ya nchi na hivyo huduma ya afya kuendelea kuimarika.
Katika kuhitimisha washiriki wa warsha hiyo waliunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi za dini katika kuboresha huduma ya afya kwa kuanzisha teknolojia hiyo mpya ya kutumia Kompyuta kwenye hospitali.
Mradi wa mfumo huo wa Kompyuta unafadhiliwa na Shirika la misaada la (CORDAID) kwa kushirikiano na shirika la Kimataifa la Mawasiliano na Maendeleo (IICD) yote ya nchini Uholanzi umeanzishwa mwaka 2006 na unamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kupitia kitengo chake cha mawasiliano kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa na takwimu sahihi za afya kwa njia rahisi, na tangu kuanzishwa kwa mfumo huo tayari baadhi ya hospitali zimeanza kutumia teknolojia hiyo, hospitali hizo ni pamoja na Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), St.Elizabeth, Seliani, KCMC, hospitali teule ya wilaya ya Ngorongoro (Wasso) na Dodoma Christian Medical Centre.
Imewekwa: 24th Nov 09 na Renatus Sona
|