|
Mkutano wa tathimini ya miradi ya IICD
Matumizi ya Kompyuta yaboresha huduma ya afya Mwanza Imeelezwa kuwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) katika sekta ya afya yamechangia kuleta mabadiliko makubwa kwa hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo tayari zimeanza kutumia mfumo mkoani Mwanza.
Hayo yamebainishwa na washiriki wa mkutano wa tathimini ya Miradi inayofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano na Maendeleo (IICD) la nchini Uholanzi.
Meneja mradi wa mfumo wa Kompyuta wa DHMIS unaotekelezwa na baadhi ya hospitali za mkoa wa Mwanza, Bw. Deogratias Kattonyella amesema tangu kuanza kwa utekelezwaji wa mradi huo hospitali za Bukumbi na Nyamagana, Vituo vya afya vya Nyakato na Makongoro na zahanati za Nyakahoja na Nassa zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma ambapo wagonjwa wamekuwa wakipata huduma kwa muda mfupi hali ambayo imechangia wagonjwa wengi kupata huduma ya haraka na isiyokuwa na msongamano.
Aidha Bw. Kattonyella amedai kuwa mfumo huo umechangia hospitali kuwa na ripoti sahihi kutokana na takwimu kuhifadhiwa katika Kompyuta.
Kwa upande wake Bi. Pauline Kimollo ambaye anasimamia mradi wa Kompyuta unaotumia mfumo wa Care2x amesema, matumizi hayo ya Kompyuta yameweza kusaidia hospitali nyingi kujua idadi ya mapato yanayokusanywa kwa siku sambamba na idadi za dawa zilizopo Stoo hivyo hakuna aina yeyote ya udanganyifu unaojitokeza katika mfumo huo.
Akizungumza katika mkutano huo mwakilishi kutoka ofisi ya mganga wa jiji Dk.Kokugonza Mugeye amesema kuwa baada ya mafanikio ya kutumia mfumo wa Kompyuta kuonekana katika hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Halmashauri ya jiji la Mwanza inategemea kuviunganisha vituo vingine 8 vya Serikali katika mfumo huo mwaka huu.
Pamoja na mafanikio hayo kupatikana, ni changamoto chache zimejitokeza katika mfumo huo ambazo ni pamoja na; tatizo la umeme kwa baadhi ya vituo vya afya, vifaa vya mfumo (Kompyuta) na kukosekana kwa mafunzo ya kutosha kwa watumishi.Miradi hiyo inayofadhiliwa na IICD ni; AfyaMtandao, DHMS (AfyaPro), HMIS (Care2x), Telemedicine, TEKNOHAMA hospitali ya wilaya ya Magu na Sengerema, e-learning.
Imewekwa: 6th Jan 10 na Renatus sona
|